TATHIMINI YA MPANGO KAZI WA KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO.

Posted on: March 31st, 2023

Timu ya Afya kutoka ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Afya pamoja na watoa huduma za Afya ya mama Na mtoto ndani ya Mkoa wa Mwanza wamekutana pamoja katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kujadili mrejesho wa mpango mkakati uliowekwa ili kupunguza vifo vya mama Na mtoto nchini.

Tathimini ya mpango kazi huu imeongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa ambae amesisitiza
kufuatilia utekelezaji wa yale yanayojadiliwa katika vikao hivi, pia utekelezaji huu uwe katika ngazi zote kuanzia Hospitali za rufaa za mikoa mpaka vituo vya Afya.

Kikao kazi hiki kimelenga kutoa mrejesho wa tathmini ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maazimio ya vikao vya kitaifa ( Zoom MPDSR) vya mapitio ya vifo vya mama Na mtoto vilivyojitokeza ndani ya Mkoa wa Mwanza kwa mwaka 2021/2022, kutathmini utekelezaji wa mpango kazi, changamoto na namna ya kuzitatua ili kuboresha zaidi huduma hizi.

Tathimini ya mpango kazi huu imefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando ikiwa ni Hospitali kuu inayoongoza kuratibu upunguzaji wa vifo vya mama na mtoto kanda ya ziwa chini ya mwenyekiti wa Huduma za afya ya mama na mtoto kanda ya ziwa ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Dkt. Fabian A Massaga.

Serikali kupitia Wizara ya afya imeendelea kuboresha Huduma za afya ya mama na mtoto nchini, kipekee katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa kuhakikisha upatikanaji wa vituo vya afya pamoja na vifaa tiba vinavyosaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.