MENO YA MTOTO YASITIKISWE YANAPOFIKIA HATUA YA KUNG’OKA

Posted on: January 2nd, 2023

Kiafya inashauriwa meno ya utotoni yanapofikia muda wa kung’oka yasitikiswe, ili kuepuka madhara mbalimbali ikiwemo kuathiri mishipa ya fahamu ya mtoto.

Kimsingi jino la utotoni ambalo kitaalam linaitwa la awali, linapolegea kwa vyovyote lipo lingine jipya linaloota chini yake, linaloitwa la kudumu.

“Kunatokea hali ya kufyonza kwenye jino jipya, ambayo husaga mzizi wa jino la awali na kulifanya lipande juu, hatimaye kung’oka lenyewe,” amesema Mtaalam wa kinywa na meno katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, Dk Casmir Kiloya.

Amesema wakati mwingine kusagika kwa mzizi huenda kusifanyike kwa usahihi, kutokana na umbali uliopo kati ya jino la zamani na jipya, hivyo kusababisha la awali kutolegea.

Matokeo yake la kudumu litachomoza pembeni mwa lile la awali, na kwa hali hiyo mzazi anashauriwa kumpeleka mtoto hospitali, ambapo jino la utotoni litaondolewa kitaalam ili kulipatia nafasi jipya kukaa panapostahili.

Amesistiza jino kutong’olewa kienyeji, kwani madhara yake ni makubwa, ikiwemo uwezekano wa mtoto kuvuja damu nyingi pamoja na kuota uvimbe pale jino lilipotolewa.

Amesema uvimbe nao ukitibiwa kienyeji utasababisha hadi kifo, amesema Dk Casmir Kiloya na kuongeza kuwa: “Lakini pia meno yakishakuwa mawili eneo moja mzazi anaweza kuondoa la kudumu na kuacha la awali, hivyo kumsababishia mtoto pengo la maisha kwa sababu hakuna tena uwezekano wa kuota jino lingine.”

Unakaribishwa katika huduma ya kinywa na meno katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou toure